HAPPY MAPINDUZI DAY! KWANINI MAPINDUZI, KWANINI MUUNGANO?

Ndugu zangu,
Usiku wa kuamkia leo, miaka 51 iliyopita, yaani, Januari 12 , 1964, na ilikuwa ni Jumapili kama hii, ndio ilikuwa Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nilikuwa Zanzibar hivi karibuni, nilipata nafasi ya kuongea na WaZanzibar. Nilidadisi Mapinduzi yale ya 1964, nilidadisi Muungano wetu.
Na tujifunze kupitia historia. Naamini, kuwa historia ni Mwalimu Mzuri sana. Maana, hatuwezi kuyajua ya leo kama hatuyajui ya jana. Na hivyo, hatutoweza kupata mwanga kwa yatakayotokea kesho.
Shuleni nilipenda sana kusoma habari za Wanamapinduzi wa dunia hii. Kusoma habari za mapinduzi ya umma katika sehemu za dunia. Habari za Mapinduzi ya Zanzibar zilinivutia sana. Nilipata kusoma kitabu cha John Okello kilichonivutia sana kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar. Kiliitwa ' Zanzibar Revolution'.
Kupitia historia hiyo nilifahamu habari za wanamapinduzi kama vile Abdurahman Babu, Edington Kissasy, Kassim Hanga na wengineo. Nilipomaliza Form Four pale Tambaza Secondary nilibahatika kufanya safari ya kwanza maishani mwangu kuvuka bahari. Safari ya kwenda Unguja.
Huko nilikuwapo wakati wa sherehe za Mapinduzi Jan 12, 1989. Nilifurahia kuwapo mahala palipokuwa na vuguvugu la Mapinduzi ya mwaka 1964. Kuviona kwa macho na kutembea kwenye vitongoji vya Zanzibar; Mkunazini, Ziwani, Fuoni, Mji Mkongwe na kwengineko.
Nakumbuka shuleni tulisoma kuwa Karume alikuwa kiongozi wa Mapinduzi yale. Taarifa hizi zinawasilishwa tofauti kulingana na mitazamo ya wenye kuziwasilisha. Ukisoma maelezo kwenye kitabu cha John Okello na hata mwandishi mahiri Ryszard Kapuchinski, kuna mtazamo wenye kutofautiana na tulichofundishwa shuleni.
Mwandishi Ryszard Kapuchinski alikuwapo Dar es Salaam na Zanzibar wakati wa mapinduzi. Kapuchinski anaandika; kuwa Karume alikuwa Dar es Salaam wakati mapinduzi yale yakiendelea kule visiwani. Kapuchinski anamzungumzia Karume kama mtu aliyekuwa akiongea kwa sauti ya juu sana hata ukikaa nae karibu. Mara nyingi Karume alikuwapo pale New Africa Hotel, mahali walipokutana wanamapinduzi wengi wa bara hili.
Ninapotafakari mitazamo tofauti juu ya dhana ya Mapinduzi ya Zanzibar, na kwa vile nimepata bahati ya kufika visiwani na kuongea na WaZazibar na wa Mji Mkongwe na wa mashambani, kuna uhalisia ninaouona, kuwa suala la Zanzibar na hususan Muungano si jepesi kama wengine wanavyofikiri, au wanavyotutaka tufikiri.
Maana, Muungano ni zao la Mapinduzi ya 1964. Yale ya 1964 yalikuwa ni Mapinduzi ya Umma. Ni Mapinduzi ya Wajamaa wa Kiafrika. Ni muhimu watu wakajua historia sahihi ya Mapinduzi, lakini, yumkini swali muhimu leo si nani aliyewaongoza wakulima, wavuvi na wakwezi wale kufanya mapinduzi, bali, kuyafahamu malengo ya mapinduzi yale na kama yamefikiwa.
Na hakika, Kuuvunja Muungano leo ni kuvunja misingi ya uwepo wa Tanganyika kama dola. Kuna hasara kidogo sana kubaki kwenye muungano, na hasara na madhara makubwa zaidi kuwa nje ya Muungano.
Zanzibar ya jana, leo na kesho, itabaki kuwa ni mkusanyiko wa wenyeji wa asili mbali mbali. Na wengi ni Waafrika wa kutokea Tanganyika. Mathalan, Zanzibar ina WaZanzibar wenye asili ya Unyamwezi, Usukuma, Umakonde, Uluguru, Uzaramo, Undengereko, Urabau, Ushiraz na kadhalika. Hivyo basi, swali gumu ni je, Mzanzibar ni nani nje ya Muungano? Unafikiri haya unapokutana na Wazanzibar wenye kuongea Kinyamwezi lakini hawajawahi kukanyaga Sikonge wala Urambo, Tabora.
Bila shaka, Mwalimu Nyerere aliposema kama ingewezekana Zanzibar isogezwe na upepo iwe mbali na Tanganyika huenda ingekuwa nafuu, naye alikuwa akisumbuliwa na ukweli huo. Kuwa ni vigumu kwa Tanganyika kuondokana na Zanzibar katika uhalisia uliopo. Tulivyo sasa, suala la Zanzibar ni letu Tanganyika, na la Tanganyika ni la Zanzibar pia.
Yalikuwa malengo sahihi, ya waasisi wa Muungano kuwa uanze na Serikali MBILI kwa lengo la kwenda kwenye Serikali MOJA. Na kuunganisha vyama; Afro Shiraz na TANU ulikuwa ni mwanzo wa safari ya kuelekea kwenye kuyafikia malengo hayo. Maana, Serikali kibaraka wa Sultan iliyopinduliwa 1964 haikuwa na malengo ya kuukomboa umma wa Zanzibar ulio na mchanganyiko wa hata wenye asili ya Bara. Serikali iliyoundwa na ZNP na ZPPP ilikuwa ni mabaki ya Usultani ambao wanyonge walio wengi visiwani hawakuwa na faida nao.
Huu ni wakati wa kujitafakari. Ni wakati wa kujisahihisha pia. Kuyaacha malengo ya waasisi ya kuufikia Muungano Kamili wa Serikali MOJA kutoka kwenye Serikali MBILI, na kubadili mwelekeo kwenda kwenye Serikali TATU, kimsingi itakuwa ni kuianza safari ya kurudi Tanganyika na Zanzibar pasipo MUUNGANO.
Ni safari ya kuuvunja Muungano wenyewe. Na kama hivyo ndivyo, ni hekima na busara jambo hilo likaamuliwa kwa kura ya maoni iliyotanguliwa na elimu juu ya faida na hasara ya maamuzi ya ama kubaki kwenye Muungano wa Serikali MBILI au kwenda kwenye Serikali TATU.
Happy Mapinduzi Day!

No comments:

Post a Comment