
Ndugu zangu,
Usiku wa kuamkia leo, miaka 51 iliyopita, yaani, Januari 12 , 1964, na ilikuwa ni Jumapili kama hii, ndio ilikuwa Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Usiku wa kuamkia leo, miaka 51 iliyopita, yaani, Januari 12 , 1964, na ilikuwa ni Jumapili kama hii, ndio ilikuwa Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nilikuwa
Zanzibar hivi karibuni, nilipata nafasi ya kuongea na WaZanzibar.
Nilidadisi Mapinduzi yale ya 1964, nilidadisi Muungano wetu.
Na
tujifunze kupitia historia. Naamini, kuwa historia ni Mwalimu Mzuri
sana. Maana, hatuwezi kuyajua ya leo kama hatuyajui ya jana. Na hivyo,
hatutoweza kupata mwanga kwa yatakayotokea kesho.
Shuleni
nilipenda sana kusoma habari za Wanamapinduzi wa dunia hii. Kusoma
habari za mapinduzi ya umma katika sehemu za dunia. Habari za Mapinduzi
ya Zanzibar zilinivutia sana. Nilipata kusoma kitabu cha John Okello
kilichonivutia sana kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar. Kiliitwa ' Zanzibar
Revolution'.
Kupitia
historia hiyo nilifahamu habari za wanamapinduzi kama vile Abdurahman
Babu, Edington Kissasy, Kassim Hanga na wengineo. Nilipomaliza Form Four
pale Tambaza Secondary nilibahatika kufanya safari ya kwanza maishani
mwangu kuvuka bahari. Safari ya kwenda Unguja.
Huko
nilikuwapo wakati wa sherehe za Mapinduzi Jan 12, 1989. Nilifurahia
kuwapo mahala palipokuwa na vuguvugu la Mapinduzi ya mwaka 1964. Kuviona
kwa macho na kutembea kwenye vitongoji vya Zanzibar; Mkunazini, Ziwani,
Fuoni, Mji Mkongwe na kwengineko.
Nakumbuka
shuleni tulisoma kuwa Karume alikuwa kiongozi wa Mapinduzi yale.
Taarifa hizi zinawasilishwa tofauti kulingana na mitazamo ya wenye
kuziwasilisha. Ukisoma maelezo kwenye kitabu cha John Okello na hata
mwandishi mahiri Ryszard Kapuchinski, kuna mtazamo wenye kutofautiana na
tulichofundishwa shuleni.
Mwandishi
Ryszard Kapuchinski alikuwapo Dar es Salaam na Zanzibar wakati wa
mapinduzi. Kapuchinski anaandika; kuwa Karume alikuwa Dar es Salaam
wakati mapinduzi yale yakiendelea kule visiwani. Kapuchinski
anamzungumzia Karume kama mtu aliyekuwa akiongea kwa sauti ya juu sana
hata ukikaa nae karibu. Mara nyingi Karume alikuwapo pale New Africa
Hotel, mahali walipokutana wanamapinduzi wengi wa bara hili.
Ninapotafakari
mitazamo tofauti juu ya dhana ya Mapinduzi ya Zanzibar, na kwa vile
nimepata bahati ya kufika visiwani na kuongea na WaZazibar na wa Mji
Mkongwe na wa mashambani, kuna uhalisia ninaouona, kuwa suala la
Zanzibar na hususan Muungano si jepesi kama wengine wanavyofikiri, au
wanavyotutaka tufikiri.
Maana,
Muungano ni zao la Mapinduzi ya 1964. Yale ya 1964 yalikuwa ni Mapinduzi
ya Umma. Ni Mapinduzi ya Wajamaa wa Kiafrika. Ni muhimu watu wakajua
historia sahihi ya Mapinduzi, lakini, yumkini swali muhimu leo si nani
aliyewaongoza wakulima, wavuvi na wakwezi wale kufanya mapinduzi, bali,
kuyafahamu malengo ya mapinduzi yale na kama yamefikiwa.
Na
hakika, Kuuvunja Muungano leo ni kuvunja misingi ya uwepo wa Tanganyika
kama dola. Kuna hasara kidogo sana kubaki kwenye muungano, na hasara na
madhara makubwa zaidi kuwa nje ya Muungano.
Zanzibar
ya jana, leo na kesho, itabaki kuwa ni mkusanyiko wa wenyeji wa asili
mbali mbali. Na wengi ni Waafrika wa kutokea Tanganyika. Mathalan,
Zanzibar ina WaZanzibar wenye asili ya Unyamwezi, Usukuma, Umakonde,
Uluguru, Uzaramo, Undengereko, Urabau, Ushiraz na kadhalika. Hivyo basi,
swali gumu ni je, Mzanzibar ni nani nje ya Muungano? Unafikiri haya
unapokutana na Wazanzibar wenye kuongea Kinyamwezi lakini hawajawahi
kukanyaga Sikonge wala Urambo, Tabora.
Bila
shaka, Mwalimu Nyerere aliposema kama ingewezekana Zanzibar isogezwe na
upepo iwe mbali na Tanganyika huenda ingekuwa nafuu, naye alikuwa
akisumbuliwa na ukweli huo. Kuwa ni vigumu kwa Tanganyika kuondokana na
Zanzibar katika uhalisia uliopo. Tulivyo sasa, suala la Zanzibar ni letu
Tanganyika, na la Tanganyika ni la Zanzibar pia.
Yalikuwa
malengo sahihi, ya waasisi wa Muungano kuwa uanze na Serikali MBILI kwa
lengo la kwenda kwenye Serikali MOJA. Na kuunganisha vyama; Afro Shiraz
na TANU ulikuwa ni mwanzo wa safari ya kuelekea kwenye kuyafikia malengo
hayo. Maana, Serikali kibaraka wa Sultan iliyopinduliwa 1964 haikuwa na
malengo ya kuukomboa umma wa Zanzibar ulio na mchanganyiko wa hata
wenye asili ya Bara. Serikali iliyoundwa na ZNP na ZPPP ilikuwa ni
mabaki ya Usultani ambao wanyonge walio wengi visiwani hawakuwa na faida
nao.
Huu ni
wakati wa kujitafakari. Ni wakati wa kujisahihisha pia. Kuyaacha malengo
ya waasisi ya kuufikia Muungano Kamili wa Serikali MOJA kutoka kwenye
Serikali MBILI, na kubadili mwelekeo kwenda kwenye Serikali TATU,
kimsingi itakuwa ni kuianza safari ya kurudi Tanganyika na Zanzibar
pasipo MUUNGANO.
Ni safari
ya kuuvunja Muungano wenyewe. Na kama hivyo ndivyo, ni hekima na busara
jambo hilo likaamuliwa kwa kura ya maoni iliyotanguliwa na elimu juu ya
faida na hasara ya maamuzi ya ama kubaki kwenye Muungano wa Serikali
MBILI au kwenda kwenye Serikali TATU.
Happy Mapinduzi Day!
No comments:
Post a Comment