Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akitoa hotuba yake wakati wa kilele cha mbio
za mwenge 2014 ziilizofanyika katika uwanja wa michezo wa Ali Hassan
Mwinyi mjini Tabora siku ya jana.GPL(P.T)
Vijana, Michezo, Utamaduni na Michezo;
Mheshimiwa Zainabu Omar Mohamedi, Waziri wa Uwezeshaji,
Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto – Zanzibar;
Mheshimiwa Fatuma A. Mwasa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora;
Mheshimiwa Samwel Sitta, Waziri wa Afrika Mashariki, Spika Mstaafu na Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi;
Ndugu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar;
Makatibu Wakuu kutoka Wizara Mbalimbli Tanzania
Bara na Zanzibar;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Waheshimiwa viongozi wa vyama mbalimbali vya Siasa;
Viongozi wetu wa Kiroho kutoka katika Madhebu mbalimbali;
Vijana Wetu;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Nawashukuru
Mawaziri wetu Mheshimiwa Fenella Mukangara wa Serikali ya Muungano na
Mheshimiwa Zainabu Omari Mohamed wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwa kunialika kuja kushiriki katika sherehe za mwaka huu za kilele cha
Mbio za Mwenge wa Uhuru. Napenda pia kutumia nafasi hii kumpongeza na
kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora na viongozi wenzake na wananchi wote
wa Tabora kwa kukubali kuwa mwenyeji wa sherehe hizi na kwa maandalizi
mazuri. Hakika sherehe zimefana sana. Tunawashukuru kwa mapokezi
mazuri na kwa ukarimu wenu.
Pongezi kwa Wizara na Wananchi
Aidha,
nawapongeza Makatibu Wakuu, viongozi waandamizi na maafisa wa ngazi
mbalimbali wa Wizara zetu mbili husika kwa kazi kubwa na nzuri ya
kuandaa na kusimamia utekelezaji wa programu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru
mwaka 2014. Matunda yake mema sote tunayashuhudia na kujivunia. Pamoja
na hao napenda kuwatambua, kuwashukuru na kuwapongeza Wakuu wa Mikoa,
Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Watendaji wa Halmashauri na viongozi wa
Shehiya, Majimbo, Kata, Vijiji na Mitaa kote nchini kwa kuziwezesha Mbio
za Mwenge mwaka huu kupita kwa usalama katika maeneo yao.
Mwisho,
lakini siyo mwisho kwa umuhimu, nawapongeza na kuwashukuru wananchi wote
kwa jinsi walivyoupokea na kuukimbiza Mwenge katika maeneo yao. Kama
tulivyosikia Mwenge umekagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwa
miradi 1,451 yenye thamani ya shilingi bilioni 361.3. Hii ni miradi
mingi yenye manufaa makubwa na kufanya mbio hizi kuwa chachu kubwa ya
maendeleo hapa nchini. Hongereni sana.
Pongezi kwa Wakimbiza Mwenge
Nawapongeza
sana vijana wetu waliokimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa chini ya uongozi
wa Ndugu Rachel Kasanda kwa kazi kubwa na nzuri ya kukimbiza Mwenge kwa
siku 165kupitia Mikoa yote, Wilaya zote, vijiji vingi na mitaa mingi
kote nchini. Poleni kwa yote yaliyowakuta lakini uvumilivu wenu na moyo
wenu wa upendo na uzalendo kwa nchi yenu ndivyo vilivyotuwezesha
kufikia kuiona siku ya leo. Mwenge mmeufikisha salama Tabora ukiwa
unang’ara kama ilivyo kawaida yake. Nawashukuru kwa Risala yenu na kwa
kunikabidhi Kitabu kikubwa chenye Risala za Utii za wananchi wa
Tanzania. Kama ilivyo ada tutazisoma zote na mambo yanayostahili
kufanyiwa kazi tutachukua hatua stahiki.
Ndugu Wananchi;
Kama
mjuavyo, katika sherehe hizi pia tunakumbuka tarehe na siku kama ya leo
mwaka 1999 ambapo mpendwa wetu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere alitutoka hapa duniani. Ilikuwa siku ya majonzi na simanzi
kubwa. Leo, hata hivyo, siyo siku ya kuomboleza, bali ni siku ya
kusherehekea maisha ya kiongozi wetu mpendwa asiyekuwa na mfano wake na
muasisi wa taifa letu lililo huru la Tanganyika, Desemba, 1961 na wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964 kwa kushirikiana na Mzee
Abeid Amani Karume.
Katika
kipindi cha uongozi wake na uhai wake Mwalimu aliifanyia nchi yetu mema
mengi ambayo daima hayatasahaulika. Hivyo basi, siku kama ya leo ni ya
kukumbuka kazi zake nzuri pamoja na mambo mengi mazuri aliyotuachia kama
urithi. Ni siku ya kutafakari na kuona namna gani tutayadumisha na
kuyaendeleza.
Sherehe
za mwaka huu ni spesheli kweli kweli, kwani zinafanyika siku chache tu
baada ya Bunge Maalum la Katiba kukamilisha kazi yake na
kukabidhi Katiba Inayopendekezwa. Katiba hiyo ambayo imepatikana chini
ya uongozi wa mwana Tabora, mashuhuri, Mheshimiwa Samwel Sitta
imesisitiza ubora na kuendelea kwa Muungano wa Serikali Mbili alizoasisi
Mwalimu Julius Nyerere akiwa na Mzee Abeid Amani Karume. Bila ya shaka
mtakumbuka jinsi Mwalimu alivyoupigania muundo huo kwa nguvu zake zote
wakati wa uhai wake. Hatuna budi kulipongeza Bunge Maalum la Katiba kwa
uamuzi wake wa busara ambao unamuenzi kwa dhati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na kudumisha urithi wake mkuu kwetu ambayo ni Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Sijui tungesema nini katika Sherehe za mwaka
huu kama ndiyo tungekuwa na Katiba Inayopendekezwa yenye muundo wa
Serikali Tatu?
Mwenge na Taifa Letu
Ndugu Wananchi;
Mwenge wa Uhuru ni moja ya alama muhimu ya umoja wa nchi yetu na utaifa
wetu. Mwenge umebeba falsafa kubwa ndani yake kuhusu nchi yetu na
uhusiano wake na watu wengine duniani hasa wanyonge wenye dhiki
wasiokuwa na amani. Wakati wa harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika
kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza Mwalimu Julius Nyerere aliwahi
kusema “Sisi tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya mlima
Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo
hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa
dharau”. Dhamira hii ilitimizwa tarehe 9 Desemba, 1961 siku Tanganyika
ilipopata Uhuru. Pamoja na kupandisha bendera ya taifa huru la
Tanganyika kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro na Mwenge wa Uhuru
uliwashwa.
Miaka michache baadaye utaratibu wa kukimbiza Mwenge ulianza na
kuendelea mpaka sasa. Mwenge wa Uhuru umeendelea kumulika nchi nzima
ukipita katika mitaa, vijiji, shehia na majimbo, wilaya na mikoa
ukieneza ujumbe wa udugu, umoja, upendo, amani na mshikamano miongoni
mwa Watanzania. Aidha, Mwenge umeendelea kuwakumbusha Watanzania wajibu
wa kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujiletea maendeleo yao na ya
nchi yetu. Pia wapige vita maovu nchini.
Kwa
kuzingatia dhima nyingine ya Mwenge wa Uhuru, nchi yetu na sisi
Watanzania tumejitolea kwa hali na mali kusaidia ndugu zetu Barani
Afrika waliokuwa wanatawaliwa kujikomboa kutoka kwenye makucha ya
wakoloni na wabaguzi wa rangi. Ni fahari kwetu kwamba wananchi wa
Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Namibia na Afrika Kusini wamepata ukombozi
na uhuru wao na sisi tumetoa mchango muhimu. Ni jambo la faraja kubwa
kwamba nchi yetu imeweza kuwapatia hifadhi ndugu zetu wa nchi jirani na
hata mbali wakati maisha yao yalipokuwa hatarini kwa sababu ya
kukosekana kwa amani au kwa kukimbia mateso ya uongozi wa kikatili na
kidikteta. Ndugu zetu wa Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya na
Comoro wanajua ukweli huo. Na, kwa Uganda tuliwasaidia kuling’oa
dikteta Idd Amin na Comoro tumewasaidia kuunganisha tena nchi yao. Hivi
karibuni ndugu zetu wa Sudani Kusini waliniomba tuwasaidie kupatanisha
makundi makuu yanayohasimiana katika Chama chao kikuu cha SPLM.
Nimekubali, hivyo tutaanzisha mchakato huo tuone tutafika nao wapi.
Ujumbe wa Mbio za Mwenge
Ndugu Wananchi;
Nimefurahishwa
sana na kuafiki ujumbe wa mwaka huu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru
unaosomeka “Katiba ni Sheria Kuu ya Nchi: Jitokeze kupiga kura ya Maoni
Tupate katiba Mpya”. Ujumbe huu ni mwafaka kabisa kwa kipindi hiki cha
mchakato wa kupata Katiba Mpya nchini. Pamoja na ujumbe huu mahususi wa
kila mwaka, Mwenge wa Uhuru umeendelea kuelimisha jamii na kutoa
msukumo kuhusu vita dhidi ya UKIMWI, malaria, dawa za kulevya na
rushwa. Nawapongeza sana Wakimbiza Mwenge kitaifa kwa kuwasilisha
ujumbe wa mambo yote manne vizuri.
Ndugu Wananchi:
Kama
mnavyofahamu nchi yetu iko katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpya.
Mchakato huu sasa umeingia hatua ya juu kabisa baada ya kumalizika kwa
Bunge Maalum la Katiba kwa kutunga Katiba Inayopendekezwa. Baada ya
Katiba Inayopendekezwa kukabidhiwa kwangu na kwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba tarehe 8 Oktoba, 2014 mjini Dodoma,
kazi inayofuata ni Kura ya Maoni ya wananchi kuamua ili nchi yetu ipate
Katiba Mpya. Hatua husika kuhusu matayarisho ya kutekeleza masharti ya
Kura ya Maoni zimeshaanza kuchukuliwa. Nawaomba Watanzania wenzangu
muwe na subira. Mtaelezwa na kuelekezwa ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimebahatika
kuisoma Katiba Inayopendekezwa na naendelea kuisoma. Kwa kweli ni
Katiba bora, kuliko hii tuliyonayo sasa yaani Katiba ya mwaka 1977. Ni
Katiba inayotambua na kuimarisha tunu za taifa letu na mambo mazuri ya
huko tulikotoka na hapa tulipo. Ni Katiba inayorekebisha upungufu
uliopo sasa na kuweka mifumo mizuri inayoendana na wakati tulionao sasa
na huko mbele tuendako. Kwa lugha nyepesi ni Katiba inayotoa majawabu
sahihi kwa changamoto zetu za leo na kesho.
Katiba
Inayopendekezwa inatokana na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa
Tanzania walioko ndani na hata wale walio nje ya nchi. Ndiyo maana haki
na maslahi ya makundi yote zimetambuliwa na kupewa nafasi yake
stahiki. Kama mjuavyo, leo pia ni kilele cha Wiki ya Vijana. Napenda
mjue kuwa Katiba Inayopendekezwa imetambua haki za vijana na kuelekeza
kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa. Kuundwa kwa Baraza hilo
kutawaongezea vijana sauti katika kushiriki kwenye utungaji wa sera na
uamuzi unaohusu maendeleo ya vijana na nchi yenu (ambayo ndiyo yetu
sote). Kitakuwa chombo huru cha kuunganisha vijana wote nchini bila
kubagua kwa jinsia, rangi, kabila, dini, ufuasi wa vyama vya siasa na
maeneo watokako katika kutafuta majawabu ya changamoto zinazowakabili
ikiwemo tatizo kubwa la ajira.
Hii ni
fursa ambayo vijana wamekuwa wakiililia tangu kutungwa kwa Sera ya
Vijana ya mwaka 1996. Hatimaye kilio hiki kimepatiwa kitambaa cha
kufutia machozi na Katiba Inayopendekezwa. Shime vijana mjitokeze kwa
wingi wakati utakapofika, mpige kura ya kuunga mkono Katiba
Inayopendekezwa ili mjitengenezee hatma njema ninyi na vizazi vyenu.
Mnayo nafasi sasa ya kihistoria ya kushika hatamu ya maendeleo yenu.
Katiba Inayopendekezwa ni fursa hiyo, hakikisheni haiwaponyoki.
Ndugu Watanzania Wenzangu;
Naomba
muisome kwa makini Katiba Inayopendekezwa ili muielewe na kuona jinsi
masuala muhimu kuhusu vijana na wananchi wengine yalivyozingatiwa.
Epukeni kuondolewa kwenye mambo yenye maslahi ya moja kwa moja na ustawi
wenu na kubeba agenda hasi za watu wengine. Kamwe msikubali kutumika
na kutumiwa na wanasiasa au wanaharakati kwa mambo ambayo hayana tija
kwenu na nchi yetu. Nawaomba vijana mtambue kuwa kwa sababu ya umri
wenu, ninyi ndiyo mtakaoishi na kufaidi matunda ya Katiba
Inayopendekezwa kwa miaka mingi ijayo. Kwa sababu hiyo, itumieni fursa
hii vizuri, kutengeneza mustakabali mwema kwenu na kwa vizazi vyenu.
Hatima ya nchi yetu iko mikononi mwenu.
Ndugu Wananchi;
Bila ya
shaka mnajua kuwa mwezi Desemba, 2014 kwa upande wa Tanzania Bara
kutafanyika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Napenda kutumia fursa hii
kuwashauri vijana na wananchi wote wenye sifa stahiki na kujitokeza
kugombea uongozi. Pia nawaomba mjitokeze kwa wingi na kushiriki kwa
ukamilifu katika kupiga Kura siku ya uchaguzi. Kufanya hivyo ndiko
kutakakotupatia viongozi wazuri wanaoweza kutuvusha na kutupeleka huko
mbele kuzuri tunakokutaka. Tushirikiane ili tupate viongozi wanaoendana
na mahitaji ya sasa na ya miaka ijayo mbele. Ngazi za kitongoji, mitaa
na kijiji ndizo ngazi za msingi za kuanzia za kuleta maendeleo na
mabadiliko katika nchi yetu.
Shughuli
za maendeleo na utoaji wa huduma za jamii hasa zinafanyika katika
vijiji, vitongoji na mitaa tunayoishi. Hivyo, mabadiliko mnayoyataka
hamna budi yaanzie katika mitaa au kitongoji unachoishi. Hii ndiyo ngazi
inayotugusa moja kwa moja kila mmoja wetu katika maisha yetu ya kila
siku. Hivyo basi, vijana mjitokeze kugombea uongozi katika uchaguzi wa
Serikali za Mitaa. Vile vile, mwakani kwenye Udiwani, Ubunge na
Uwakilishi, msibaki nyuma. Ni haki yenu na ni wakati wenu. Gombeeni
hata kwa nafasi ya Urais, na iwapo kuna mtu anayefanana na ujana na
atakuwa ametimiza masharti ya Katiba, asiogope, ajitokeze. Watu
wataamua. Shime jitokezeni mkawe chachu ya mabadiliko katika maeneo
mnayoishi na nchi nzima.
Wiki ya Vijana
Ndugu Wananchi;
Kama sehemu ya sherehe hizi, jana nilitembelea Kijiji cha Mfano cha
Vijana katika wilaya ya Sikonge. Nimefurahishwa sana na juhudi
zifanywazo na vijana za kujiletea maendeleo. Nimevutiwa na miradi
mbalimbali wanayoitekeleza pale ikiwemo ya kufuga nyuki na kuvuna mazao
yatokanayo na nyuki, ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa, ushonaji nguo
na viatu. Halikadhalika, shughuli za kilimo na ujenzi wa nyumba bora.
Nimewashauri viongozi wa Wilaya, Mkoa na Wizara waangalie uwezekano wa
kuwafanya vijana hao kuwa wakaazi na wamiliki wa eneo hilo la miradi ili
kiwe kweli kijiji cha mfano badala ya kuwa mahali pa kupita mithili ya
chuo cha mafunzo ya amali.
Baadae
nitapata nafasi ya kutembelea mabanda ya maonesho ya kazi wafanyazo
vijana na wadau wengine hapa uwanjani. Maonyesho haya yanathibitisha
kwa uwazi fursa zilizopo za kuwaendeleza vijana. Lililo muhimu kufanya,
ni kwa vijana kuwa na upeo mzuri wa ufahamu wa mambo, ubunifu, moyo wa
kujituma na kufanya kazi kwa bidii. Mkifanya hivyo tutaondokana na
tatizo la ukosefu wa ajira na umaskini kwa vijana na taifa kwa ujumla.
Ndugu Wananchi;
Kwa
kutambua ukweli huu, ndiyo maana Serikali zetu zimeongeza bajeti katika
Mifuko ya Maendeleo ya Vijana kupitia Wizara zetu mbili zinazosimamia na
kuratibu maendeleo ya vijana. Shabaha yetu ni kuwawezesha vijana wengi
zaidi kupata mikopo na kuwa na mitaji ya kutekeleza miradi yao
itakayowawezesha kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato. Naikumbusha
Wizara inayosimamia na kuratibu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuhakikisha
kwamba fedha za Mfuko huo zinawafikia walengwa na, kwa wakati muafaka.
Kwa
upande mwingine nazikumbusha Halmashauri zote za Wilaya na Miji
kutekeleza kwa ukamilifu agizo la kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa
mwaka kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya Vijana na Wanawake. Ninazo
taarifa kuwa baadhi ya Halmashauri zinalitekeleza vizuri agizo hili
lakini zipo nyingine ambazo zinasuasua. Nataka isiwepo hata Halmashauri
moja ya kunyooshewa kidole kwa kutokufanya vizuri kwa jambo lenye
manufaa kwa vijana wetu kama hili. Naomba nitumie nafasi hii leo
kuzitaka Halmashauri zote kutoa taarifa za mara kwa mara za utekelezaji
wa agizo hili. Taarifa ya kwanza kwa ajili hiyo itolewe mwisho wa mwezi
Desemba, 2014, ifuatayo iwe miezi minne baadae na kila baada ya miezi
minne.
Mapambano Dhidi ya UKIMWI
Ndugu Wananchi;
Janga
la UKIMWI bado ni tatizo kubwa nchini hivyo ni sahihi kabisa kwa Mwenge
kuendelea kulisemea. Inakadiriwa kuwa tunao wagonjwa wa
UKIMWI milioni 1.4. Bahati mbaya waathirika wengi zaidi ni vijana.
Takwimu za maambukizi zinaonyesha pia kuwa wasichana wa umri wa miaka 20
– 24 wako katika hatari ya kuambukizwa karibu mara tatu ikilinganishwa
na wavulana wa umri huo huo.
Ni jambo
la kutia moyo kwamba kiwango cha maambukizi kinashuka mwaka hadi mwaka
kutokana na shughuli za uhamasishaji ambazo na Mwenge nao una mchango
wake. Kwa mfano, kiwango cha maambukizi kimeshuka kutoka asilimia
5.7 mwaka 2010 hadi asilimia 5.1 mwaka 2012. Kiwango cha maambukizi ya
UKIMWI hapa mkoani Tabora ni wastani waasilimia 5.1 ambayo ni sawa na
kiwango cha kitaifa. Mwelekeo huu kwa taifa na Tabora ni mzuri lakini
tusibweteke bali tuongeze bidii katika mapambano. Watu watano katika
kila100 kuwa wameambukizwa ni wengi mno. Isitoshe maambukizi
mapya 78,843 ni makubwa mno, tunataka maambukizi mapya yawe sifuri.
Tumeendelea kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya
UKIMWI. Idadi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wanaopata tiba
imeongezeka kutoka 201,181 (2005) hadi 512,555 mwaka 2013. Hali
kadhalika tumewezesha huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto kutolewa karibu katika Kliniki zote nchini (aslimia 97).
Vilevile, idadi ya waliopima afya zao imeongezeka kutoka
watu 365,189 mwaka 2005 hadi 20,469,241 mwaka 2013. Katika mwaka 2013
peke yake, watu 2,793,636 walipima afya zao. Yote hayo ndiyo
yanayochangia kupungua kwa maambukizi.
Ndugu Wananchi;
Ili kushinda vita hii hatuna budi kukumbushana kuachana na tabia na
mienendo inayowaweka wanaadamu katika hatari ya maambukizi. Mimi
naamini Watanzania tunaweza kabisa kushinda vita dhidi ya UKIMWI.
Kinachotakiwa ni kuamua kukataa kupata maradhi haya. Inawezekana,
timiza wajibu wako.
Mapambano Dhidi ya Rushwa
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea
na mapambano dhidi ya rushwa na mafanikio yanaendelea kupatikana. Watu
wengi zaidi hivi sasa wakiwemo vijana, wamefikiwa na kampeni ya
kuwafanya watambue madhila yake, waichukie rushwa na wawe tayari
kujitokeza kupambana na uovu huu. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) imeongeza kasi ya kupambana na rushwa. Katika kipindi
cha Julai 2013 hadi Juni, 2014 imefanikiwa kufungua kesi mpya 327, kati
ya hizo kesi tatu ni za rushwa kubwa. Aidha,shilingi bilioni
38.96 zimeokolewa. TAKUKURU sasa imekwenda mbali zaidi na kuanzisha
ofisi za Waratibu wa Kanda (Public Expenditure Tracking System – PETS
Coordinators) wenye jukumu la kufuatilia matumizi ya fedha kwenye
shughuli za ununuzi hasa kwenye miradi ya maendeleo.
Tumefanya
hivyo kwa kutambua kuwa shughuli za ununuzi kwenye Halmashauri na
Serikali Kuu kwa jumla ndiko waliko mchwa wengi, wakubwa na wanene.
Katika kipindi cha 2013/14 pekee, miradi 215 yenye thamani ya
shilingi bilioni 20.594 imekaguliwa. Kati ya miradi hiyo, miradi yenye
thamani ya shilingi bilioni 9.59 ilionekana kuwa na mazingira ya mashaka
na uchunguzi wa kina unaendelea hivi sasa. Itakapothibitika kuwepo kwa
dalili za rushwa, hatua zipasazo za kisheria zitachukuliwa bila ya
ajizi.
Ndugu Wananchi;
Tunaweza kupata ushindi mkubwa zaidi katika vita dhidi ya rushwa na
mafanikio tunayoendelea kupata ni ushahidi wa ukweli wa kihistoria.
Sisi katika Serikali tutaendelea kutekeleza wajibu wetu kwa kuiwezesha
TAKUKURU kwa rasilimali watu, vitendea kazi na majengo. Mwaka huu pekee
tumeiwezesha Taasisi kuajiri Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi
Wasaidizi 304 ili kuimarisha utendaji katika taasisi yetu hii muhimu.
Tunachohitaji ni ushirikiano wa karibu wa wananchi katika kuwafichua
wale wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Ukweli ni
kwamba watu hao tunaishi nao katika maeneo yetu. Tuache kuwatukuza na
kuwalinda kwani kwa kufanya hivyo tunawaimarisha, na kuwakatisha tamaa
watu waadilifu na wale walio mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya
rushwa. Tuyachukue mapambano dhidi ya rushwa kuwa ni yetu sote na siyo
ya TAKUKURU au viongozi peke yao. Ushindi dhidi ya rushwa ni ushindi
wetu sote. Hali kadhalika, kushindwa vita dhidi ya rushwa ni kushindwa
kwetu sote. Ni hasara kwako na taifa kwa jumla.
Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tunaendelea
na mapambano dhidi ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Tunaendelea kupata mafanikio pamoja na ugumu uliokuwepo katika mapambano
hayo. Wahalifu wamekuwa wakibadili mbinu na kuongeza nguvu kila
kukicha. Hata hivyo, na sisi tumekuwa na unyumbufu wa kutosha. Ukweli
ni kwamba kadri wahalifu hao wanavyoongezeka na ndivyo wanavyoongezeka
kukamatwa. Wakati katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka 2013
walikamatwa watuhumiwa 2,000,mwaka huu tangu Januari, hadi kufikia
Oktoba, (2014) watuhumiwa 6,875wameshakamatwa na kesi zao ziko katika
hatua mbalimbali. Takwimu hizi zinaonyesha namna tulivyoongeza nguvu na
tunavyofanikiwa katika juhudi zetu.
Katika
Mkoa wa Tabora peke yake, washitakiwa 177 wamefikishwa Mahakamani.
Kilichonisikitisha zaidi ni taarifa kuwa sasa kilimo cha bangi
kinaongezeka kwa kasi mkoani Tabora. Nawaomba muendelee kuwa wakulima
hodari wa tumbaku pekee na siyo kilimo cha bangi.
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea
kuchukua hatua nyingi madhubuti kukabiliana na mtandao wa uuzaji na
usafirishaji wa dawa za kulevya, ndiyo maana taarifa za matukio ya
kukamatwa watu katika viwanja vyetu vya ndege zimepungua sana tofauti na
mwanzo mwa mwaka huu. Hii inaashiria kuwa mambo yamekuwa magumu kwenye
njia hiyo, lakini tunajua wanatafuta au watatafuta njia nyingine. Kwa
yote mawili hawatafika mbali, mkono mrefu wa sheria utawafikia.
Tumeendelea
kutoa huduma za kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya kuacha kutumia
dawa hizo na kurejea katika maisha ya kawaida. Vituo vyetu vya
majaribio katika hospitali za Muhimbili, Mwananyamala na Temeke sasa
vinahudumia waathirika wapatao 1,835 kwa kutumia dawa ya Methadone.
Tanzania ni moja kati ya nchi chache sana Afrika ambazo zimepiga hatua
kubwa katika kutibu waathirika wake na wenzetu sasa wanakuja kujifunza
kwetu. Tutafanya zaidi ya tufanyavyo sasa. Nia yetu ni kueneza huduma
hiyo nchi nzima ili kunufaisha vijana wetu wengi.
Ndugu Wananchi;
Tunayo kila sababu ya kushinda vita hii. Hatamu ya ushindi wetu iko
mikononi mwa wananchi wa Tanzania na vijana ambao ndiyo waathirika na
wateja wakubwa wa dawa hizo. Kataeni kuwa mawakala wa biashara hii
haramu na ya maangamizi. Pia kataeni kuwa watumiaji wa dawa za
kulevya. Biashara hii haiwezi kushamiri iwapo hapatakuwepo na mawakala
na wateja wa uhakika. Sisi Serikalini tunaendelea kuchukua hatua
stahiki. Sasa tunapitia upya sheria ili tuweze kuanzisha taasisi mpya
yenye mamlaka makubwa ya kupambana na dawa za kulevya kuliko Tume ya
Kudhibiti Dawa za Kulevya iliyoko sasa. Maandalizi yamefikia pazuri.
Tutakamilisha jambo hili mapema iwezekanavyo.
Maji na Barabara
Ndugu Wananchi;
Kabla ya
kumaliza naomba niwathibitishie wananchi wa Mkoa wa Tabora kwamba ahadi
yangu ya kuleta maji mjini Tabora, Nzega na Igunga kutoka Ziwa Victoria
iko palepale. Tumechelewa kuanza kutokana na kuendelea kutafuta fedha
za kutekeleza dhamira yetu hiyo. Nafurahi kusema kuwa Mungu ni mwema
tumefanikiwa. Serikali ya India imekubali maombi yangu na watatukopesha
kiasi cha dola za Marekani milioni 264 kwa ajili ya kutekeleza mradi
huu. Wataalamu wanamalizia michoro ya mradi ili baada ya hapo ujenzi
uanze. Subira yavuta heri, wote tuwe wavumilivu.
Tunaendelea
na jitihada za kujenga barabara mbalimbali kwa kiwango cha lami hapa
Mkoani Tabora. Barabara zinazoendelea kujengwa zitakamilishwa na zile
zinazoendelea na maandalizi zitaanza pindi tutakapopata fedha. Lengo
letu ni kuunganisha Mkoa huu na Mkoa wa Katavi, Kigoma na Singida
kupitia Itigi hadi Manyoni. Tumezungumza na Kuwait Fund ili watusaidie
kujenga barabara ya Nyahua – Chaya wamekubali. Hali kadhalika, Benki ya
Maendeleo ya Afrika wanaelekea kuwa tayari kutupatia mkopo wa ujenzi wa
barabara ya Tabora - Sikonge – Koga - Mpanda.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Narudia
tena kuwashukuru wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine kufanikisha
sherehe hizi ambazo zimefana mno. Baada ya kusema hayo natamka rasmi
kwamba shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu zimefikia
kilele chake leo.
Nawatakia kila la kheri katika shughuli zenu za kila siku.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment