WATU wawili wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha ya kivita
aina ya SMG, wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi, wakati
wakitaka kupora fedha kwenye duka la wakala wa Kampuni ya Bia Tanzania
(TBL), Kipipa Millers.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Christopher
Fuime, majibizano hayo ya risasi yalitokea juzi katika eneo la Igoma
wilayani Nyamagana jijini Mwanza, baada ya watu hao wanaosadikiwa kuwa
majambazi kutaka kupora fedha kwenye ghala hilo la kuuza bia.
Akifafanua juu ya tukio hilo, Kamanda Fuime alisema polisi walifika
mapema eneo la tukio, baada ya kupata taarifa za siri kwa njia ya simu,
zikieleza kuwapo kwa uhalifu wa kutumia silaha eneo la Igoma.
Alisema majambazi hao wakiwa na silaha ya kivita, bunduki aina ya Sub
Machine Gun (SMG) yenye namba za usajili JC 027014998 na panga moja,
walivamia ghala hilo la bia na kumlazimisha muuzaji kuwapa fedha za
mauzo.
Kwa mujibu wa Kamanda Fuime, muuzaji wa duka hilo, Joyce Temu (23)
baada ya kushurutishwa atoe fedha, aliamua kujificha chini ya kaunta na
kuwapa wakati mgumu majambazi hao kupitisha mtutu wa bunduki na kufyatua
risasi.
Fuime alisema kabla ya kufanya uvamizi huo, waliwalazimisha
wafanyakazi wa ghala hilo kulala nchini, ndipo wakaingia ndani, kabla ya
wananchi kujitokeza na kuwakurupusha.
Baada ya majambazi hao kukurupushwa, walikimbia kwa miguu kwenda
Kisesa huku wakipiga risasi hewani hovyo, ambapo njiani walijaribu
kumpora pikipiki dereva mmoja, lakini walishindwa kutokana na kuandamwa
na wananchi wakishirikiana na polisi.
Alidai walipoona hivyo, walilazimika kukimbilia kwenye majaruba ya
mpunga kwenda Nyamhongh’olo katika Manispaa ya Ilemela, ambapo
waliendelea kujibizana kwa risasi na polisi kabla ya kuzidiwa katika
mapambano hayo na kuuawa katika eneo la Nyamhong’olo manispaa ya
Ilemela.
Alisema bunduki iliyokuwa ikitumiwa na majambazi hao ilikuwa na
magazini mbili zenye risasi 60, lakini zilikutwa risasi 20 huku maganda
matatu wakiyaokota kwenye eneo la tukio na jambazi moja lilitoroka
katika mazingira ya kutatanisha.
Katika tukio hilo, baadhi ya wananchi walijeruhiwa kwa kupigwa risasi
sehemu mbalimbali za mwili, ambapo aliwataja kuwa ni pamoja na Lazaro
Mwakefu (25) aliyejeruhiwa chini ya goti na Petro John (35), dereva,
yeye amejeruhiwa mkono wa kushoto na wote wamelazwa Hospitali ya Rufaa
ya Bugando.
Wengine ni fundi magari, Haji Haji, mkazi wa Kigoma ambaye alipigwa
kisogoni na amefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Sekou Toure na
kuondolewa kichwa cha risasi moja.
Pia, wananchi wawili walijeruhiwa wakati wakiwafukuza majambazi hao
baada ya kuanguka, ambao ni Godfrey Nsumba aliyepata majeraha mguu wa
kulia na Lutaigwa Boniphace, yeye ameteguka mguu. Wote wamelazwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
No comments:
Post a Comment